Home KITAIFA CEO MPYA AWAPA YANGA JEURI YA KUTIKISA CAF

CEO MPYA AWAPA YANGA JEURI YA KUTIKISA CAF

0

ANDRE Mtine ametambulishwa rasmi kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa Yanga mbele ya Waandishi wa Habari na Rais wa Yanga Injinia Hersi Said

Lakini habari kubwa zaidi inayowapa jeuri mashabiki wa Yanga ni namna kigogo huyo alivyochangia kwa kiasi kikubwa kwenye harakati za TP Mazembe kuwa tishio Afrika tena mbele ya klabu nyingi kutoka mataifa ya Kaskazini yanayozungumza lugha ya Kiarabu.

Wanaamini kuwa wasifu na uzoefu wake katika kuisimamia TP Mazembe hadi ikafanikiwa kimataifa utaisadia Yanga kufanya vizuri katika mashindano ya Klabu Afrika ambayo mara nyingi imekuwa haifanyi vizuri hasa ikikwama mara kwa mara mbele ya timu kutoka Kaskazini.

Kinachowapa imani zaidi ni historia ya Mazembe kuzisumbua timu nyingi kubwa Afrika na kupata mafanikio katika miaka ya hivi karibuni, ambayo wanaamini Mtine amechangia kwa kiasi kikubwa kwani alikuwa ni miongoni mwa maofisa waandamizi wa timu.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 12 ambacho Mtine ameitumikia Mazembe, timu hiyo imetwaa mataji saba (7) ya mashindano ya klabu Afrika ambapo kati ya hayo, mawili ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mawili ya Kombe la Shirikisho Afrika na mengine matatu ni mataji ya Super Cup.

Ukiondoa mataji hayo, imemaliza katika nafasi ya pili mara tatu huku ikikwamia katika hatua ya nusu fainali mara tatu.

Katika mataji hayo saba ambayo wamechukua ndani ya kipindi ambacho Mtine alikuwepo kwenye usimamizi wa timu, mataji matano walichukua kwa kuwafunga waarabu katika mechi za fainali huku fainali mbili tu ndio walipayta taji kwa kuzifunga timu kutoka kwingineko.

Mwaka 2010 walitwaa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwafunga Esperance ya Tunisia katika fainali na mwaka 2015 walifanya hivyo kwa kuwachapa USM Alger ya Algeria na mwaka uliofuata wakatwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwafunga MO Bejaia katika fainali.

Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2017 waliifunga Supersport United ya Afrikia Kusini huku kwenye taji la Super Cup, mwaka 2010 waliifunga Stade Malien ya Mali kwenye fainali wakati mwaka 2011 na 2016 walizifunga FUS Rabat ya Morocco na Etoile du Sahel ya Tunisia mtawalia.

Mtine alitangazwa rasmi juzi kuchukuwa nafasi ya Senzo Mbatha ambaye aliachana na klabu hiyo baada ya mkataba wake kumalizika huku yeye akisaini mkataba wa miaka miwili.

Mtine alisema: “Nina uzoefu mkubwa na kazi nimefanikiwa kupita sehemu mbalimbali ikiwemo kuwa kwenye uongozi wa Shirikisho la Soka Zambia na pia nimewahi kufanya kwenye klabu ya Zesco ya Zambia pamoja TP Mazembe ya DR Congo hivyo najua nilichokuja kukifanya.

“Nimekuja kutimiza malengo ya Yanga kiu yangu ni kuona Yanga ikifika mbali na kujulikana kimataifa jambo ambalo nalitamani pia. Yanga ni timu kubwa sana, nimekuwa naifuatilia kwa muda sasa. Nimejifunza kuwa ni timu kubwa, na tunaweza kuifanya kuwa kubwa zaidi, siyo tu ukanda wa Afrika Mashariki bali kuwa klabu kubwa zaidi Afrika.” Miongoni mwa majukumu ya Mtime ni kusimamia uamuzi wa klabu ili ufanyike kama ulivyoamuliwa na kupitishwa katika vikao vya ndani vya bodi au mkutano mkuu wa klabu.

Pia anakuwa kiunganishi kati ya pande zote mbili hususani kufikia maendeleo ndani ya Yanga katika malengo yake ya muda mfupi na muda mrefu.

Kazi ya pili ni kusimamia operesheni zote, kuhakikisha wanatetea makombe yote na kufanya vyema Afrika.

ISHU YAKE

Kuhusu madai yaliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii jana jioni kwamba aliwahi kukutwa na kashfa ya utakatishaji fedha na kufungiwa maisha kujihusisha na soka kwao, Yanga jana walitoa nakala za Chama cha Soka cha Zambia na Mahakama za nchi hiyo zikionyesha kwamba alisafishwa baada ya kukosekana na hatia katika madai hayo ya miaka ya nyuma.

Hata hivyo, jana jioni walikuwa kwenye kikao kizito cha kiutendaji ambacho wote walikuwa bize na hawakuwa tayari kutoa ufafanuzi zaidi ya vielelezo hivyo.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here