Katika makala iliyopita siku ya jana tuliona Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said aliweka bayana namna klabu hiyo inavyotumia fedha katika kusuka kikosi kipya na mipango ya kuongeza udhamini zaidi klabuni. Ameweka bayana juu ya tetesi na mijadala iliyopo mtaani na mtandaoni kwamba Yanga na TFF haziivi…Ebu endelea naye…!
YANGA NA TFF
“Hauwezi kuwa na uongozi ambao unaendesha mpira bila kuwa na mahusiano mazuri, mpira wa sasa hivi una mikono mikubwa sana, kuna wenzetu kutoka klabu mbalimbali tunapaswa kushirikiana nao, kuna wenzetu wa TFF tunatakiwa kushirikiana nao, kuna bodi ya ligi, kuna baraza la michezo kuna wizara ambayo ndio serikali, azma yangu ni kuhakikisha Yanga inajenga mahusiano mazuri na taasisi zote hizi na zingine.
“Unaweza kuona jinsi tulivyo na mahusiano mazuri na jamii, klabu hii imekuwa karibu kila mchezo tunatoa ushirikiano na jamii mbalimbali kwa misaada kwa wenye uhitaji na mambo mengine, changamoto hazikosekani nikiri zipo, rapsha zinaweza kuwepo kidogo kwa kuwa hii ni klabu ya watu wengi kwa kuwa kila mtu ana mtazamo wake.
“Sisi kama viongozi tunapaswa kulibeba hili jambo kwenye uhalisia wake na kutafuta suluhisho, haliwezi kupatikana kama watu mtashindwa kukaa na kuweka mambo sawa, niseme tu kwangu mimi suala la mahusiano ni muhimu sana siwezi kuendesha hii klabu peke yangu, lazima tuwe na mahusiano yenye afya na taasisi zingine na hii ndio hatua ambayo itatufanya tuwe na mafanikio.
“Nikuhakikishie kwamba pamoja na minong’ono mingi ambayo inaendelea mimi kwangu sijawahi kuona utofauti ambao upo kati yetu na shirikisho na naamini viongozi wenzangu pia hali iko hivyo kama kwangu na hata TFF nao siamini kama wana tofauti na sisi Yanga, hatujafika eneo ambalo tunaweza kusema Yanga ina shida na shirikisho, changamoto zinazotokea za kiutendaji sisi kama viongozi ni jukumu letu kukaa chini na kuzipatia majibu..
USAJILI WA AZIZ KI
Moja ya mastaa ambao walitingisha katika usajili wa dirisha kubwa lililopita waliotua ndani ya Yanga basi alikuwa ni mshambuliaji Stephane Aziz KI.
Hersi ndiye aliyesimamia usajili huu kuanzia mwanzo mpaka mwisho hapa anaeleza jinsi Yanga ilivyopigana vita ya kuinasa saini ya mshambuliaji huyo wa zamani wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
“Malengo yalikuwa ni kuanza kuwa na kikosi imara kushinda msimu uliopita, kuelekea msimu huu na timu yetu ilikuwa na matarajio ya kuingia katika mashindano ya Kimataifa, kwahiyo tuliona uhitaji wa kuwa na wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya Kimataifa, Aziz mwaka jana kwa maana ya msimu alifanya vizuri sana akiwa na timu yake ya ASEC Mimosas tulimuona mara kadhaa hapa na kwao akifanya vizuri,” anasema Hersi.
“Tuliona iko haja kutafuta wachezaji bora kama hao watakaokuja kutusaidia, kwahiyo nilianza kumfuatilia mapema Aziz na pia baada ya kuja hapa alipokuja kucheza dhidi ya Simba kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho, tukaanza kutumia muda kumfuatilia na baada ya hapo nikajiridhisha kwamba anatufaa (Aziz KI) kwamba anaweza kuja kutusaidia.
“Nilianza kufanya mawasiliano naye ya moja kwa moja kuanzia Machi au Aprili mwaka huu, hatua ya kwanza nilimtembelea kuweka mambo sawa lakini pia nilikwenda kukutana naye nje ya nchi eneo ambalo alikuwa anacheza mechi na baada ya hapo kukawa na ugumu mkubwa nikaamua kupitia njia nyingine.
“Nikafanikiwa kumfikia mama yake ambaye alikuwa na mchango mkubwa kwenye kumsimamia mchezaji (Aziz KI), tukatengeneza mahusiano naye mazuri na kuwa naye karibu na mwisho wa siku haikuwa tu timu iliyompa kiasi kikubwa kumsajili bali ilikuwa ni timu ambayo ilimfanya kuwa salama kwake kusajiliwa hapo.
“Tuliweza kuweka mazingira mengi sawa, bahati mbaya Aziz alishawahi kupitia mazingira ya kutapeliwa alivyochukuliwa huko nyuma kutoka kwao Ivory Coast kwenda Hispania kwa klabu ya Rayo Vallecano baadaye akapata shida na kwenda Ufaransa kisha baadaye akaenda klabu ya Cyprus (Nea Salamina), hivyo alipita kwenye mikono ya watu ambao sio waaminifu, mazingira hayo yalimfanya kuwa makini kuhakikisha yaliyomtokea nyuma hayajirudii tena.
DILI LA MAYELE
“Moja katika maeneo ambayo ni muhimu sana ni kuhakikisha kwamba kama timu inafanya vizuri, kwanza usirudi nyuma kutokana na kiwango chako, ili usirudi nyuma naana yake usiachane na wale wachezaji wako ambao ni muhimu kwenye timu yako hili lilikuwa kipaumbele namba moja kwetu kabla ya kwenda kumsajili mchezaji mpya, anasema Hersi huku akiendelea kueleza.
“Ilianza kumuongezea mkataba Bakari Mwamnyeto, tukamwongezea Farid Mussa, Zawadi Mauya, Kibwana Shomari, hawa wote ni wachezaji wa kikosi cha kwanza na ni wachezaji ambao walikuwa na msaada mkubwa kwa timu ili usiwapoteze. Tukahamia kwa Djuma Shaban, Yannick Bangala na baadaye tukamwongeza Fiston Mayele wachezaji wote hawa ni wale muhimu katika kikosi cha kwanza na bado tunaendelea kwa wengine ambao muda wao ukifika nao tutawaongeza mikataba mazungumzo yao yakikamilika.
“Fiston kulikuwa na ofa nyingi kubwa sana na kiukweli kama kuna jambo ambalo naweza kulihadithia hata kwa masaa matatu ni hili suala la Fiston, kwetu sisi Yanga Fiston Mayele hakuwa mchezaji ambaye tnaweza kumuuza kwa kiasi chochote, ipo klabu ilishafika mpaka dola milioni moja ( zaidi ya Bilioni 2), kulikuwa na klabu nyingi zingine hata tunacheza nazo Ligi ya Mabingwa Afgrika msimu huu nisingependa kuzitaja, ilifika mpaka huko na sio tu hizo fedha walitaka mpaka kutupa mchezaji na fedha, kuna mchezaji nisingependa kumtaja jina, mchezaji huyo tulipewa tukiambiwa chukueni hii bilioni moja na huyu mchezaji, ingawa huyu mchezaji alikwenda klabu nyingine akitumika kama beki wa kati lakini sisi tulipewa bure.
Hatukugoma kumuuza Fiston kwa ubaya, jambo zuri lilikuwa sisi pia tulikuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji yake, hatukubakiza hapa kwa kumzibia rizki yake, kile ambacho alikuwa anakihitaji “Tukumbuke wakati Fiston anakuja alikuwa ni mchezaji wa kawaida kwa maana ya jina lake hakuwa na makuu lakini ndani ya mwaka mmoja akapokewa vizuri, hiyo, fikra za namna hiyo unampa mchezaji ziweze kuingia kwenye akili yake. Hizi tulizofanya zilikuwa ni mbinu..