Singida Big Stars iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu ikitoka Ligi ya Championship kwa jina la DTB, imeuwasha moto kwelikweli hadi sasa ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo ikila sahani moja na vigogo zikiwa timu pekee tano za ligi hiyo ambazo hazijaonja vipigo hadi sasa.
Wachezaji wanaoibeba timu hiyo ni Wabrazili watano, lakini wanne kati yao kila mmoja ameshafunga bao na kuiweka pazuri, lakini habari Za Ndaani Kabisa, zinasema kuwa nyota hao wanaishi maisha ya ki-VIP flani hivi kulinganisha na wachezaji wenzao wakiwamo wazawa.
Habari za kuaminika kutoka kambi ya timu hiyo zinasema nyota hao wamekuwa wakiishi kishua zaidi na kupewa ulinzi kiasi kwamba sio rahisi hata kuwasogelea tofauti na ilivyo kwa wachezaji wengine wakiwamo wenzao wa kigeni na wale wa wazawa ambao inadaiwa wapo mbali nao kambini.
“Hawa jamaa buana hata ukitaka kuwasogelea ufanye kazi kwani wanalindwa na hata maisha yao yapo kivyao vyao hotelini,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya timu hiyo ya mkoani Singida.
Wabrazili waliopo kwenye kikosi hicho ni Dario Frederico, Rodrigo Figueiredo, Peterson Da Cruz, Bruno Gomes na Biemes Carno ambaye ni beki wa kati akiwa ndiye pekee hajafunga bao hadi sasa, pia yumo Muargentina Miguel Escobar ambaye naye anaishi ki-vip kama Wabrazili hao.
Hakuna kiongozi yeyoye wa klabu hiyo aliyepatikana kufafanua juu ya maisha ya kipekee kwa nyota hao wa Latini Amerika, ila baadhi ya wachezaji wamefichua za Ndaani Kabisa kwamba wenzao wanaishi kivyaovyao japo wanashirikiana vizuri tu mazoezni na hata uwanjani kuipania timu hiyo.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE