Msemaji wa Klabu ya Yanga ambaye amefungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujihusisha na masuala ya soka ndani na nje ya nchi kwa miaka miwili, Haji Manara amesema kuwa anafikiria kuachana kabisa na masuala ya soka akidai kuwa wapo baadhi ya viongozi ndani ya Shirikisho hilo wameapa kumshusha.
Manara amesema ikiwa ni siku moja baada ya kutembelea Bungeni Dodoma ambapo wabunge walionyesha shauku ya Manara kutaka arudishwe kwenye kazi yake.
“Nilivyokuwa Dodoma nilipata amani kubwa sana kuona viongozi wakubwa (Wabunge) wa pande zote yaani Simba na Yanga kupiga kelele bungeni wakati vikao vya bunge vikiendelea wakipaza sauti zao Haji Manara aachiwe huru.
“Binafsi nilifarijika sana jana viongozi wangu wa Yanga, mwanasheria wangu walikutana na viongozi wa TFF kujadili suala langu la kukata rufaa. Lakini cha ajabu leo nimepokea simu na meseji lutoka kwa watu watano ndani ya TFF wakinambia Haji rufaa yako haitaweza kufanikiwa kwani wamepanga kwenda kukazia hukumu yako FIFA kabisa.
“Kwa hali hii sasa tulipofikia sioni tena sababu ya kushindana na watu ambao wameapa kabisa kwa kusema lazima wanishushe hadhi yangu. Binafsi nimetengeneza jina langu brand yangu kwa gharama kubwa sana sasa siwezi kukubali kuona taswira yangu inachafuliwa kisa mpira.
“Nipo Katika mazungumzo na familia yangu nataka niachane kabisa na mpira ili Mambo yangu mengine yaendelee.Najua Kuna watu wengi wanalipwa na watu ambao nawajua ili waandike tu habari za kunichafua mimi.
“Kuna watu hata nilivyokuja Yanga walijiapiza sitafanya kazi kwa Uhuru na Kama mnakumbuka Kwenye dabi yetu ya mwisho watu waliandika makala ya kunigombanisha na Yanga kwa kusema nimekwenda hotelini ambapo Simba waliweka kambi eti nimeenda kutoa siri”
“Sasa watu wamejiapiza leo kwenda FIFA kukazia hukumu yangu ndio ujue watu wanataka kuona Haji Manara anadondoka ili waje wafurahi. Napata amani sana kwa sasa haswa kutoka kwa mashabiki wa Yanga kwa kuwa karibu nami kwa kunitia moyo na viongozi wangu wanavyonipigania kurudi kazini.
“Binafsi sitawaacha kabisa Yanga hadi mwisho wa maisha yangu hapa duniani nitakuwa nao bega kwa bega hata kama nitakaa pembeni na masuala ya football,” amesema Manara.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE