Home KITAIFA SOKA LA BONGO KUMIMINIWA NEEMA ZAIDI NA CAF

SOKA LA BONGO KUMIMINIWA NEEMA ZAIDI NA CAF

0

Kuingia kwa Simba na Yanga katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kunaiweka Tanzania katika nafasi kubwa ya kuendelea kuingiza idadi kubwa ya timu katika mashindano ya klabu Afrika msimu ujao.

Ikiwa timu hizo mbili zitafanikiwa kuingia katika hatua ya makundi, Tanzania itakuwa na nafasi kubwa ya kuingiza klabu nne katika mashindano hayo kama ilivyofanya msimu huu na ule uliopita kwani kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa alama za Tanzania katika mfumo wa ukokotoaji wa alama za ushiriki wa mashindano ya klabu Afrika unaofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)

Nchi 12 ambazo zina alama nyingi katika mfumo huo, zinapata fursa ya kuingiza klabu nne kila moja ambapo mbili ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine mbili katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika chati ya sasa ya mfumo huo wa Caf, Tanzania inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 30.5 na iwapo Simba na Yanga zitafuzu hatua ya makundi maana yake alama ilizonazo zinaweza kuongezeka na kuifanya isogee juu zaidi ya pale ilipo sasa.

Tanzania ina nafasi kubwa ya kuzishusha Libya na Guinea ambazo ziko juu yake katika chati ya sasa, kwani nchi hizo kila moja imeingiza timu moja katika raundi ya kwanza ya mashindano hayo.

Kwa Simba na Yanga kutinga raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Tanzania inaungana na nchi nyingine tisa (9) ambazo kila moja imeingiza timu mbili katika raundi hiyo ya mwisho kabla ya ile ya makundi.

Nchi hizo tisa ni Morocco ambayo timu zake Raja Casablanca na Wydad Casablanca zimeingia raundi ya kwanza, Misri (Al Ahly na Zamalek), Afrika Kusini (Mamelodi Sundowns na Cape Town City), Tunisia (Esperance na Monastir), DR Congo (TP Mazembe na AS Vita Club), Angola (Petro Luanda na Primiero de Agosto), Sudan (Al Hilal na Al Merrikh), Nigeria (Rivers United na Plateau) na Algeria ambayo imeingiza CR Belouizdad na JS Kabylie.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here