Viongozi wa Geita Gold wako kwenye wakati mgumu baada ya mshambuliaji wao, Miraj Athuman ‘Sheva’ kugomea mazoezi kwa kile kinachodaiwa kutokamilishiwa fedha zake zote za usajili (signing fees) alizoahidiwa mwanzo.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai nyota huyo anadai kiasi cha Sh3 milioni alizoahidiwa ila ameshindwa kupewa kwa wakati kwani viongozi hao waliwekeza nguvu zaidi kwa kiungo wao mshambuliaji, Said Ntibazonkiza.
Taarifa za uhakika zinadai kuwa Ntibazonkiza aliyejiunga nao baada ya kumalizana na Yanga alitaka aingiziwe fedha zake zote za usajili walizokubaliana ndipo viongozi wakaamua kuachana kwanza na Sheva ili wakamilishe usajili wa staa huyo.
Akizungumza Mwenyekiti wa timu hiyo, Leonard Bugomola alishindwa kuweka wazi juu ya taarifa hizo huku akisema yapo mambo madogo ambayo wao kama viongozi wanayashuhulikia na kila kitu kitakuwa wazi.
Kwa upande wa Sheva hakutaka kulizungumzia hilo huku akisema ameomba uongozi wake kwenda nyumbani kwa siku tatu ili kutatua changamoto zake za kifamilia.
Hata hivyo viongozi wa Geita wanapambana usiku kucha ili kumpatia staa huyo fedha zake ili kuepuka yaliyowakuta msimu uliopita baada ya kumsajili Ditram Nchimbi na kushindwa kumtumia kwa sababu kama hizo.