Vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanaendelea kujifua jijini Dar es Salaam huku wakijipanga kucheza mechi zisizopungua mbili wakati huu wa mapumziko ya ligi hiyo, lakini taarifa tamu ziwafikie mashabiki wa klabu hiyo ni kurejea tena uwanjani wa kiungo fundi, Khalid Aucho ‘Dokta’.
Aucho aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa Septemba 13 akitumika kwa muda usiozidi dakika 30 na nafasi yake kuchukuliwa na Zawadi Mauya na kumfanya akose mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini ambapo Yanga ilishinda mabao 5-0 na kuvuka raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 9-0.
Hata hivyo, kiungo kutoka Uganda ameshusha presha kwa benchi la ufundi baada ya kurejea tena mazoezi kuungana na wenzake, ikiwa siku moja tu tangu nyota wengine wawili waliozua hofu kwa mashabiki, Fiston Mayele na Bernard Morrison kujiunga na wenzao wakitoka kwenye majeraha.
Licha ya Mayele, BM33 na Aucho kurejea, mambo si mambo kwa kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kwani ataendelea kuwa chini ya uangalizi wa daktari kutokana na kupewa muda wa mapumziko.
Akizungumza daktari wa timu ya Yanga, Shecky Mngazija alisema baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina wamebaini shida ya Aucho imeisha ndio maana ameungana na wenzake, ila kwa Fei Toto bado ataendelea kuwa nje kwa muda wakimsikilizia kwanza.
“Utimamu wa miili kwa wachezaji ni mkubwa shida ni mfululizo wa mechi za michuano na wamekuwa wakitumika kila mara na kusasababisha kushtua enka na nyama za paja na hiyo inaweza ikawa sababu,” alisema Dk Mngazija na kuongeza;
“Majukumu yangu ni kuwapatia dawa kuwapunguzia maumivu, ila hali zao zimetengamaa na sasa wanafanya mazoezi hadi muda wa mechi ya michuano watakuwa timamu zaidi.”
Mngazija alisema kipindi hiki cha mapumziko amepewa jukumu la kuhakikisha anawafanyia vipimo wachezaji wote na kumkabidhi kocha wa viungo. Meneja wa timu hiyo, Walter Harrison akizungumzia kikosi, alisema kinaendelea ratiba ya mazoezi chini ya kocha msaidizi Cedric Kaze na wanafanya mpango wa kucheza mechi za kirafiki.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE