HUKU kwa sasa akielekeza akili yake katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara ugenini dhidi ya Ihefu FC, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema siku 10 zinamtosha kukiandaa kikosi chake kuhakikisha kinafanya vizuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Yanga baada ya kuitoa Zalan FC ya Sudan Kusini katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 9-0, raundi ya kwanza sasa itaanzia nyumbani dhidi ya Al Hilal iliyoitoa St. George ya Ethiopia kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2.
Al Hilala ilikubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini kabla ya kushinda nyumbani kwa bao 1-0, hivyo kunufaika na bao la ugenini, wakati Yanga yenyewe ilishinda mchezo wa kwanza mabao 4-0 na kisha wa marudiano kuibuka na ushindi wa 5-0, shukran kwa straika wao hatari, Fiston Mayele aliyetupia mabao sita kwa kufunga hat-trick katika kila michezo yote miwili.
Tayari Yanga wameanza mazoezi ya utimamu wa mwili ‘gym’ pale Gymkhana jijini Dar es Salaam kabla ya leo kuanza mazoezi ya uwanjani kwa ajili ya michezo hiyo wakitaka kwanza kumalizana na Ihefu FC Septemba 29 na kisha Ruvu Shooting Oktoba 3, mwaka huu kabla ya kuialika Al Hilal tano baadaye.
Kocha Nabi alisema kabla ya kuvaana na Ruvu Shooting, watakuwa wamefanya mazoezi magumu ambayo yatawapa majibu kuelekea katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Alisema mazoezi ya gym yatawasaidia wachezaji wake kuongeza stamina na kuwapa uwezo wa kupambana kwa dakika zote 90, kufanyia kazi mapungufu aliyoyaona kwenye mechi zilizopo.
“Nimeandaa programu maalum kwa wachezaji wangu, matarajio yangu siku 10 kuanzia leo hadi siku ya mechi, wachezaji watakuwa imara, hasa safu ya ushambuliaji kuwa makini kwa nafasi wanazozipata katika mechi,” alisema Nabi.
Alisema wachezaji wake hawajapata muunganiko mzuri hivyo anahakikisha anaendelea kutengeneza taratibu kikosi chake na kupata matokeo mazuri katika michezo iliyopo mbele yao ikiwamo dhidi ya Ihefu na Ruvu Shooting na kisha dhidi ya Al Hilal Oktoba 8, mwaka huu.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE