Wapinzani wa Simba Agosto ya Angola watawasili jijini Dar es Salaam Oktoba 14 kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya kugombania kufuzu hatua ya makundi ya kombe la Washindi barani Afrika.
Mechi hiyo itachezwa Jumapili Oktoba 16.
Msemaji wa Simba Ahmed Ally amesema wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo na rasmi wameanza mazoezi leo katika uwanja wa Bunju uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
“Tulishinda lakini bado hatujafuzu, safari hii hatutaki kurudia makosa. Tumeweka nguvu kubwa kuona kwamba mchezo wa jumapili tunapata matokeo mazuri ili tuingie makundi,”
“Tumemiss kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.”
“Tutaendelea kuwakosa Shomari Kapombe ambaye sasa anaendelea kufanya mazoezi akiwa hospitali, ataukosa mchezo wa jumapili lakini michezo itakayofuata atakuwepo,” amesema Ally.
Ally amesema Jimmyson Mwinuke pia ataukosa mchezo huo, lakini taarifa njema ni kuwa Peter Banda amerejea kikosini.
“Wageni wetu Primeiro de Agosto watawasili nchini Oktoba 14 majira ya mchana, kwa wale ambao wangependa kwenda kuwapokea wanakaribishwa uwanja wa ndege,”
” Waamuzi wanatokea Afrika Kusini na watawasili nchini siku hiyo hiyo ya Oktoba 14,” amesema.
“Upande wa hamasa tunaendelea kupita kwenye vyombo vya habari na kupita mitaani, siku ya ijumaa tutakuwa Temeke, tutazunguka na kispika twende tukaiunge mkono timu yetu,”.
” Tukio la kipekee tutakuwa na chakula cha pamoja, biryan la kwenda hatua ya makundi.”
“Siku ya mchezo milango itafunguliwa mapema, kutakuwa na burudani kabla ya mchezo.
“Tutagawa bendera uwanja mzima kwa kila shabiki wa Simba jukumu lake ni kupeperusha. Lengo letu ni kutengeneza hali ya kuvutia uwanjani ili ionekane ni mechi ya Simba.”
Kuhusu kocha Juma Mgunda, ally amesema
“Kocha Mgunda anafanya vizuri na kila mmoja anaona. Simba tuliyokuwa tunaitaka tunaiona kwake. Namna watu wanashambulia, wanavyokaba na mpira unavyotembea. Bodi ya Wakurugenzi itafanya maamuzi lakini ametupa tunachotaka na tunaamini atatupeleka makundi.”
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE