Kocha wa klabu ya Kipanga ya Zanzibar Hamis Hassan ameitaka klabu ya Yanga kuwa makini na wapinzani wao katika kombe la Shirikisho klabu ya Africain ya Tunisia.
Kocha Hassan amesema klabu hiyo ni nzuri sana katika eneo la kiungo na ni timu shindani ambayo sio ya kubeza.
Kipanga ilitoka sare na Africain katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo ya vilabu barani Afrika katika mechi iliyochezwa Zanzibar.
Lakini wakiwa Tunisia, walifungwa 7-0 katika mechi hiyo ya marudiano ya kombe la Shirikisho.
‘”Ni timu ambayo inaichukulia michuano hii kwa umakini sana,”
” Inatumia mfumo wao wa 4-4-2 ambao sio mgeni katika mpira , ila wana wachezaji wazuri katika eneo la kiungo,”
” Kwa mechi ya hapa nyumbani Yanga wakiwa makini wapinzani wao wanafungika vizuri sana,”
” Sisi tulishindwa kuwafunga kwa sababu hatukuwa na uzoefu wa michuano mikubwa,”
” Lakini pia hatuna wachezaji wanaoweza kuamua mechi,”
” Ila Yanga wana aina hiyo ya wachezaji , hivyo wakijipanga vizuri wanafungika, ila sio wa kubeza,” amesema wakati akihojiwa na Capital Radio.
” Ila ni wagumu sana wanapokuwa nyumbani kwao Tunisia ,” amesema.
Klabu ya Yanga SC imepangwa dhidi ya Club African ya Tunisia katika droo ya hatua ya mwisho ya mtoano ya kombe la Shirikisho
Yanga SC itaanzia nyumbani Dar es Salaam mnamo Novemba 2, 2022 kabla ya kurudiana Novemba 9, 2022.
Yanga imeangukia katika kombe la Shirikisho baada ya kutolewa katika michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika na Al Ahilal ya Sudan.
Yanga imetolewa katika klabu bingwa kwa matokeo ya jumla 2-1.