Home KITAIFA KUELEKEA MAKUNDI CAF, HIZI HAPA REKODI ZA MNYAMA

KUELEKEA MAKUNDI CAF, HIZI HAPA REKODI ZA MNYAMA

0

Simba inasubiri Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lipange droo ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Novemba ili kujua itaangukia kwenye kundi gani na wapinzani wake watatu watakuwa kina nani.

Makala haya inakuletea mafanikio ya Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika tangu 2013 na kile ilichokifanya katika michuano hiyo yenye fedha nyingi inayokutanisha miamba ya soka la Afrika.

2013

Hapa ndipo Simba ilikuwa inaanza kupashapasha kwenye michuano hiyo mikubwa yenye fedha nyingi. Iliishia hatua ya awali baada ya kufungwa jumla ya mabao 5-0 dhidi ya Recreativo do Libolo ya Angola na kuacha maneno mengi mitaani kwa mashabiki.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza Februari 17, 2013 wababe hao wa Msimbazi wakiwa nyumbani Uwanja wa Mkapa walifungwa bao 1-0.

Marudiano uliopigwa Machi 3, 2013 kwenye Uwanja wa Estadio Municipal de Calulo ambapo ilifungwa mabao 4-0. Ngoma ikaishia hapo.

2018

Baada ya kutoshiriki mashindano ya kimataifa kwa muda msimu wa 2016-17 kwenye mashindano ya ndani ilichukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa kuifunga Mbao FC mabao 2-1 mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. Baada ya ushindi huo iliwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika na iliwaondoa Gendarmerie Nationale kwa mabao 5-0 baada ya mechi zote mbili.

Katika mechi ya kwanza Simba ilishinda mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Mkapa wakati ile ya marudiano Gendarmerie ikiwa nyumbani Djibout ilifungwa bao 1-0. Simba iliondolewa kwenye hatua ya pili kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya Al- Masry ya Misri kwani katika mechi ya kwanza Uwanja wa Mkapa mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 wakati ule wa marudiano uliisha kwa suluhu. Bado Simba ikaendelea kujifunza.

2018-19

Tangu ilivyoondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali 2013, Simba haikushiriki mashindano ya kimataifa hadi msimu wa 2018-19. Msimu huo ulikuwa wenye rekodi kwa Simba baada ya kutinga robo fainali ilikoondolea na TP Mazembe ya DR Congo. Simba ilianzia hatua ya awali ikikutana na Mbabane Swallows na mechi ya kwanza Mnyama akiwa Uwanja wa Mkapa, Novemba 28, 2018 ilishinda mabao 4-1.

Mechi ya marudiano ikiwa Eswatini Desemba 4, 2018 ilishinda mabao 4-0. Baada ya hapo ilicheza hatua ya pili ikianzia ugenini dhidi ya Nkana ya Zambia ilikofungwa mabao 2-1 mjini Kitwe na wiki moja ilirudiana na wakali hao wa Zambia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Desemba 23, 2018 ilikuwa siku ya kihistoria kwa Simba baada ya kushinda mabao 3-1 na kutinga hatua ya makundi – mabao ya Simba yakifungwa na Jonas Mkude, Meddie Kagere na Clatous Chama. Baada ya ushindi dhidi ya Nkana Red Devils ilitinga makundi ilikopangwa kundi D na timu za Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na AS Vita ya DR Congo.

Katika hatua ya makundi ilianzia nyumbani dhidi ya JS Saoura ikishinda mabao 3-0 yaliyofungwa na Meddie Kagere aliyetupia mawili na Emmanuel Okwi. Simba ilikutana na vipigo viwili vizito ambapo Kinshasa ilifungwa 5-0 na AS Vita na idadi kama hiyo ilifungwa na Al Ahly huko Misri. Baada ya vipigo ilirejea nyumbani kucheza na Al Ahly ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Kagere. Simba ilikwenda ugenini Algeria kwa JS Saoura na kufungwa mabao 2-0.

Timu hiyo ilicheza mechi ya mwisho ya kundi nyumbani dhidi ya AS Vita na ilihitaji ushindi ili itinge robo fainali na mchezo huo ulimalizika kwa Mnyama kushinda mabao 2-1 akitokea nyuma kwa bao moja na mabao yake yakifungwa na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Clatous Chama.

Katika robo fainali Simba ilianzia nyumbani dhidi ya TP Mazembe – mchezo uliomalizika kwa suluhu wakati ule wa marudiano ilifungwa 4-1, huku ikianza kupata bao kupitia kwa Emmanuel Okwi.

2019-20

Licha ya mafanikio msimu uliopita katika mashindano hayo msimu 2019-20 ulikuwa mbaya kwake kwani iliondolewa hatua ya awali kwa kanuni ya bao la ugenini matokeo ambayo hayakutegemewa na wengi.

Timu hiyo iliondolewa na UD Songo ya Msumbiji ambapo ikiwa ugenini mechi iliisha kwa suluhu wakati mchezo wa marudiano kwa Mkapa ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 na UD Songo ikitangulia kufunga kupitia Luis Miquissone kabla ya Erasto Nyoni kusawazisha. Msimu huo ulikuwa mchungu kwa Simba kutokana na wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutotegemea iwapo chama lao lingekwama kutokana na mafanikio liliyopata msimu uliotangulia.

2020-21

Huu ulikuwa msimu wa mafanikio kwa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikianzia hatua ya pili lakini iliondolewa robo fainali na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Kwenye hatua ya pili ilianzia ugenini dhidi ya Platinum ya Zimbabwe ikafungwa bao 1-0 wakati nyumbani – kwa Mkapa ilishinda abao 4-0 na kutinga hatua ya makundi. Mnyama alipangwa kundi A na Al Ahly, AS Vita na El Merrikh ya Sudan.

Msimu huo ilionyesha ubora ikimaliza ya kwanza kwenye kundi nyuma ya miamba ya soka la Afrika – Al Ahly iliyoshika nafasi ya pili. Kwenye mechi sita za makundi Simba ilishinda nne, sare moja, ikafungwa moja ambapo ilifunga mabao tisa ikifungwa miwili na kukusanya pointi 13.

Simba ilianzia ugenini dhidi ya AS Vita ikishinda bao 1-0, ikarudi kwa Mkapa na kushinda 1-0 dhidi ya Al Ahly, ikaenda Sudan kwa Al Marreikh ikatoka suluhu. Baada ya hapo ilirudi nyumbani kucheza mechi mbili mfululizo dhidi ya Al Merreikh iliyoifunga mabao 3-0 na AS Vita iliyokula kichapo cha mabao 4-1, wakati mchezo wa mwisho ilicheza ugenini Misri dhidi ya Al Ahly na kulala kwa bao 1-0.

Katika hatua ya robo fainali, Mnyama alianza vibaya mchezo wa ugenini baada ya kufungwa mabao 4-0 na Kaizer Chiefs nchini Afrika Kusini, lakini wiki moja baadaye walirudiana na wapinzani hao kwa Mkapa na kushinda mabao 3-0 matokeo ambayo yaliyowaondoa kwenye mashindano hayo.

2021-22

Katika msimu huu Simba ilifanya vibaya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuondolewa kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana ambayo katika mchezo wa kwanza ilishinda mabao 2-0 ugenini wakati mchezo wa marudiano nyumbani ilikubali kufungwa mabao 3-1, licha ya kuanza ikiwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Rally Bwalya dakika 45 kipindi cha kwanza.

Baada ya kushuka Kombe la Shirikisho Afrika ilicheza mechi mbili za mtoano dhidi ya Red Arrows ya Zambia – mchezo wa kwanza ukipigwa kwa Mkapa na Simba ikashinda mabao 3-0 wakati ule wa marudiano ilifungwa 2-1.

Mnyama alipangwa kundi D katika hatua hiyo dhidi ya RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na USGN ya Niger. Kwenye hatua ya makundi ilimaliza katika nafasi ya pili na kupata nafasi ya kutinga robo fainali katika michezo sita ilikoshinda mitatu, sare moja na kupoteza miwili ikikusanya pointi 10 sawa na vinara – RS Berkane, lakini tofauti ilikuwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba ilicheza mechi ya kwanza nyumbani makundi ikashinda mabao 3-1, ikaenda ugenini dhidi ya USGN na kupata sare ya bao 1-1, lakini baada ya hapo ilifungwa mabao 2-0 ugenini na RS Berkane. Baada ya hapo ilirudi nyumbani na kumfunga RS Berkane bao 1-0 na ilicheza mechi ya mwisho ugenini na Asec Mimosas na kufungwa mabao 3-0, wakati mchezo wa mwisho hatua ya makundi ulimalizika kwa Mkapa ikitoa kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya USGN. Simba ilitinga robo fainali na ilianzia nyumbani ikishinda bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates wakati mchezo wa ugenini Afrika Kusini ilipoteza kwa idadi hiyo ya bao na mechi kwenda hatua ya penalti.

Simba iliondolewa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa penalti kwenye zile tano ikipata tatu na kukosa mbili wakati Orlando Pirates ilipata nne na kukosa moja. Nini maoni yako kuhusiana na ushiriki wa Simba msimu huu

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here