Home KITAIFA MGUNDA AKISAKA REKODI MPYA, PHIRI NAE KUMBE ANAJAMBO LAKE

MGUNDA AKISAKA REKODI MPYA, PHIRI NAE KUMBE ANAJAMBO LAKE

0

Kikosi cha Simba kimeondoka alfajiri ya leo kwenda Angola kuwahi pambano la awali ya raundi ya kwanza la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao, Primiero do Agosto, huku nyota wa timu hiyo, Moses Phiri akisema ana jambo lake huko.

Simba na Agosto zitavaana Jumapili kwenye Uwanja wa 11 de Novembro, huku Phiri na nyota wengine wa kikosi hicho wakionekana kuwa na mzuka mkubwa wa kupata matokeo bora kabla ya kurejea hapa nyumbani kumaliza kazi.

Kinara huyo wa mabao wa Simba, akiwa na mawili katika michuano ya CAF na manne ya Ligi Kuu Bara, alisema wanajua wana mchezo mgumu ugenini huku wakikabiliwa na rekodi mbaya iliyowekwa timu hiyo nchini humo ilipofungwa 4-0 na Recretivo de Libolo mwaka 2013.

Phiri alisema yeye na wachezaji wote wanachokiangalia ni kuwapa heshima wapinzani wao ili kuanza kwa matokeo mazuri ugenini kabla ya kumaliza kazi katika mchezo wa marudiano wiki ijayo itakayoamua hatua ya kutinga makundi ya ligi hiyo ama kuangukia Kombe la Shirikisho.

Phiri alisema kuna kazi kubwa ya kupambana na kujitolea kwa wachezaji ambao watapata nafasi ya kucheza katika mchezo huo kwani kwenye mashindano hayo sio rahisi kupata matokeo bora hasa unapokuwa mbali na nyumbani.

“Tumeelezwa mara ya mwisho kucheza Angola ilikuwa ni 2013 dhidi ya Libolo na tulipoteza kwa mabao mengi katika raundi kama hii, ila msimu huu hatutaki kuliona hilo linatokea tena.

“Tunaenda kupambania matokeo mazuri na kufuta rekodi mbaya huko Angola jambo ambalo litaturahisishia katika mchezo wa marudiano hapa nyumbani,” alisema Phiri na kuongeza;

“Tunafanya yote hayo ili kufikia malengo yetu ya kufuzu katika hatua ya makundi na hilo linawezekana kutokana na kikosi chetu kilivyo pamoja na aina ya wapinzani ambao tunakutana nao.”

Winga machachari, Pape Ousmane Sakho alisema msimu uliopita Simba haikufanya vizuri katika michuano hiyo kwenye hatua kama hii ambayo wanakwenda kucheza dhidi ya Agosto kwa nia mbili kupata matokeo mazuri na kujiweka pazuri na pia kulipa kisasi dhidi ya miamba hiyo ya Angola.

Sakho alisema kila mchezaji aliye kambini ana hamu na morali ya hali ya juu kuona wanapata matokeo bora katika mechi hiyo ya ugenini ila kuja kumaliza kazi hapa nyumbani.

“Mechi hizi za ugenini zinakuwa na changamoto kubwa ila kama tuliweza kushinda ugenini kwenye hatua ya awali dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi basi hata hapa inawezekana kufanya hivyo kwani kila mchezaji anakwenda kupambana hadi mwisho,” alisema Sakho aliyechukua tuzo ya bao bora la mshindano hayo msimu uliopita na kuongeza;

“Wachezaji tukipambana na kila mmoja akafanya vizuri kwa nafasi yake nikuhakikishie tunakwenda hatua ya makundi bila kuzuia chochote kwani mechi zote mbili tutapata matokeo bora.”

Mshambuliaji Augustine Okrah alisema kuna kazi kubwa mbele yao ili kufikia malengo ya kufika hatua ya makundi kutokana na aina ya wapinzani ambao wanaenda kucheza nao tena ugenini.

“Unajua mechi hizi za ugenini katika mashindano haya zinakuwa na mambo mengi ila Simba tunahitaji kuonyesha ukubwa wetu katika mchezo huo wa ugenini hata kama tutashindwa kushinda basi tusipoteze,” alisema Okrah, huku kiungo, Nelson Okwa alisema msimu uliopita Simba iliishia hatua hiyo ila msimu huu hawatamani kuona jambo hilo linatokea kutokana maandalizi ya kutosha ambayo wameyafanya kabla ya mechi yenyewe.

“Naamini kikosi chetu ni bora kuliko chao,” alisema.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here