KIKOSI cha timu ya taifa ya vijana U23 ina jambo zito leo Kwa Mkapa. Mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya kuwania fainali za Afcon 2023, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ akitamba kwamba jeshi lake lipo tayari kuvaana na Nigeria leo kwa Mkapa.
Mshindi wa mechi baina ya timu hizo atasonga mbele kwenye raundi ya tatu na ya mwisho ya kuwania nafasi saba za kwenda Morocco kwenye fainali za Afcon U23 ambazo pia zitatoa wawakilishi wa Afrika katika Michezo ya Olimpiki ya 2024.
Alikiri kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu na yenye ushindani, lakini kwa namna alivyoiandaa timu ana uhakika wa kupata matokeo mazuri nyumbani kabla ya kwenda kurudiana na wapinzani wao, ili kusonga mbele.
Timu hiyo ya Tanzania ilitinga hatua hiyo baada ya kuiondosha Sudan Kusini katika mechi za raundi ya kwanza kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya 0-0 nyumbani na 3-3 ugenini, mchezo ukipigwa nchini Rwanda.
“Wachezaji wapo tayari, wengi wamesharipoti kambini na wapo fiti, jambo zuri walipita katika timu za miaka 17 na 20 ambazo ni sehemu sahihi kwa vijana, wachezaji wangu wananipa moyo,” alisema Morocco, nyota wa zamani wa kimataifa wa Tanzania akitokea Zanzibar aliyewahi kuzinoa timu za Coastal Union, Namungo na timu za taifa, Taifa Stars na Zanzibar Heroes.
Juu ya wapinzani wao (Nigeria), Morocco alisema anajua ni timu ngumu lakini na yeye ana kikosi chenye wachezaji wazuri ambao wanaweza kumpa matokeo.
“Tuna mechi ngumu na Nigeria na tunajua wana timu nzuri lakini sisi pia tupo vizuri na mpira ni mchezo wa uwanjani,” alisema Morocco.
Nigeria ina rekodi nzuri dhidi ya Tanzania kwani Juni mwaka 2011 katika mechi ya kuwania Michezo ya Olimpiki ya 2014, zilikutana na Tanzania kushinda nyumbani 1-0 kabla ya kulala ugenini 3-0 na kutolewa.
Katika siku za hivi karibuni Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika michuano kadhaa iliyohusisha timu mbalimbali za vijana jambo ambalo wadau wamesifia kwamba ni mwanzo mzuri.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE