Home KITAIFA HUYU HAPA MTZ ALIYETOBOA BILA SIMBA NA YANGA, KUTOKA KUCHEZA CHANDIMU MPAKA...

HUYU HAPA MTZ ALIYETOBOA BILA SIMBA NA YANGA, KUTOKA KUCHEZA CHANDIMU MPAKA KUSAJILIWA NNJE YA NCHI

0

Achana na kijana Majaliwa (20) jasiri aliyewaokoa baadhi ya abiria katika ajali ya ndege kule Bukoba na akapewa ofa ya kwenda kusomea uokoaji, sasa kuna mwingine katika soka aliyepata zari la mentali, baada ya kutokata tamaa.

Kwa kawaida mchezaji anayecheza Ligi Kuu ndiye mwenye nafasi ya kuonekana na timu za nje, ila imekuwa tofauti kwa Maximilian Assenga (24), amesaini mwaka mmoja kuichezea Ethiopian Medhin ya Ligi Kuu ya Ethiopia, akitokea timu ya mtaani ya Malkia FC ya Kariakoo.

Kipaji cha soka hakifichiki, ndicho kilichotokea kwa winga huyu baada ya kukiwasha kitaa, hakujua kama Mungu anamfungulia milango ya kutimiza ndoto zake za kucheza soka kwa mafanikio makubwa.

Katika mahojiano yake na gazeti la  Mwanaspoti anafunguka “Kabla ya kusaini Ethiopian Medhin zipo timu nyingi za hapa nyumbani ambazo zilihitaji huduma yangu, ila nikaona ngoja nisipuuze bahati ya kutoka,” anasema.

Japokuwa hakutaka kuzitaja timu hizo, Mwanaspoti linatambua timu zilizomfuata ni Ken Gold ya Championship, KMC na Mwadui FC.

Winga huyo ambaye aliwahi kuzitumikia Panone, Machava, Friends Rangers, huku timu yake ya mwisho ikiwa ni Malkia FC ya Kariakoo,anasema alifanya majaribio katika timu kama Azam FC na Coastal Union licha ya kukubalika, ila kulitokea sababu zilizo nje ya uwezo wake.

“Historia ya maisha yangu ndiyo iliyonifanya nipate moyo wa ujasiri wa kutokukata tamaa, mama yangu mzazi alifariki nikiwa na miezi sita, nimelelewa na mama mdogo, Merry Mushi, mara zote aliniambia anatamani kuniona natetea kipaji changu, hivyo maneno yake yalikuwa kama tiba kwangu.

“Tumezaliwa watatu kwa mama, nina dada zangu wawili wa kwanza Magreth, Doreen, hao pia walikuwa wananiambia tunakutegemea, hayo ndio yakanifanya nisikate tamaa kupambania kipaji changu.”

Assenga anakubali aina ya uchezaji wa Clatous Chama wa Simba, anasema licha ya kucheza kwa nidhamu timu yake ya mtaani, pia alijitafutia biashara ya kuongeza kipato cha kujikimu kimaisha.

“Katika biashara zangu ninazozifanya, nilikuwa najitoa sana kwa timu nyingine za mtaani, maana kiukweli napenda sana soka lipo kwenye damu yangu, niliamini ridhiki yangu ikinifikia nitaipata,”anasema.

USAJILI WAKE

Hakutaka kumtaja Mtanzania aliyefanikisha dili lake, akisaidiana na wakala wa nje, baada ya kumuona akicheza mtaani alimpigia simu na kumwambia kuna watu wamemuona na wanahitaji huduma yake.

“Nakumbuka baada ya kutoka kwenye mechi, nilipigiwa simu na Kocha David Mayonga akaniambia kuna watu watakutafuta, kweli nikapokea namba ya mtu mzito tu kwenye soka la Tanzania akaniambia kuna ofa hii, watu wamependa kipaji chako, sikuamini kwa uharaka hadi nilipoonana nao na kusaini mkataba huo,”anasema.

Anasema kwa kuwa alikuwa anaamini ndoto zangu ana kila kitu anachopaswa kuwa nacho mchezaji kama paspoti ya kusafiria, hivyo ikifika Desemba anatakwenda kujiunga na timu yake mpya.

Anamtaja staa wa zamani wa Simba na Yanga, Haruna Moshi ‘Boban’ alikuwa anamtia moyo na kumwambia ana kipaji, kabla ya kupata timu itakayomtambulisha anapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia nidhamu.

“Kuna wakati alikuwa ananipitia nyumbani na kwenda naye mazoezini, akinitazama alikuwa ananiambia riziki ipo mikononi mwa Mungu siku ikifika sitapata tabu kuipata, kweli nimeipata na nitamtafuta nimwambie utabiri wake umetimia,”anasema.

Kocha Mayonga ambaye alimfundisha Assenga tangu akiwa shule hadi timu hiyo ya mtaani, anasema ni mchezaji asiyekata tamaa mbali na kipaji ana nidhamu ya juu, kutekeleza majukumu yake.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here