Nabi alifaulu hapa
Upangaji wa kikosi kilichoanza katika mchezo wa juzi ulionyesha wazi kuwa Yanga haikutaka kuingia kinyonge katika mchezo ule na ilipania kuwashangaza wenyeji jambo ambalo lilitimia.
Nabi alifanya mabadiliko matatu katika kikosi chake kilichocheza mchezo wa kwanza ambao ulimalizika kwa sare tasa hapa Dar es Salaam ambapo ukiondoa Djuma Shaban aliyebakia nchini kutokana na majeraha ambaye nafasi yake ilizibwa na Joyce Lomalisa, Nabi aliwaanzisha Ducapel Moloko aliyechukua nafasi ya Tuisila Kisinda na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye alianza badala ya Stephane Aziz Ki.
Yanga walivuja jasho hasa
Ni mchezo ambao kila mchezaji wa Yanga alionekana kutimiza wajibu wake ndani ya uwanja na pengine ni vigumu kuteua mchezaji bora wa mechi kwa upande wao jana.
Yanga walikimbia kilomita nyingi pindi walipokuwa na mpira na pale ambapo hawakuwa nao, walishinda mipira mingi ya pili walipowania na wachezaji wa Club Africain, walikuwa na nidhamu ya juu ya kulinda na kushambulia na hawakuwapa mwanya wapinzani kuleta madhara langoni mwao.
Kuthibitisha hilo, hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika, Club Africain walipiga shuti moja tu lililolenga lango ambalo walipata katika dakika za mwisho za kipindi hicho.
Sure Boy, Diarra hatari
Kama kuna watu ambao watabakia vichwani mwa wachezaji wa Club Africain basi ni kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kipa Djigui Diarra na mshambuliaji Bernard Morrison.
Kiwango bora katikati mwa uwanja cha Sure Boy katika kuichezesha, kuisogeza timu mbele kwa haraka na kupiga pasi zilizofikia walengwa kwa usahihi, kilitibua mipango mingi ya Club Africain.
Diarra na Morrison waliwatoa mchezoni wachezaji wa Club Africain mara kwa mara jambo lililowaondolea utulivu wapinzani wao na kushindwa kuwa na hatari kwao katika dakika nyingi za mechi.
Refa hana baya
Mwamuzi Issa Sy wa Senegal alizitafsiri vyema na kwa haki sheria za mpira wa miguu na hakutoa aina yoyote ya upendeleo kwa timu zote mbili.
Licha ya wenyewe kutaka kumhadaa mara tatu tofauti refa huyo ili awazawadie pigo la penalti, Sy alisimama imara na kutoingia katika mtego wa wachezaji wa Club Africain. Matokeo hayo yameifanya Yanga kuweka rekodi ya kibabe Arabuni ambayo imekuwa nadra kwa timu za Afrika Mashariki.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE