Home KITAIFA KISA YACOUBA AIDHA MAKAMBO AU KISINDA KUSEPA YANGA

KISA YACOUBA AIDHA MAKAMBO AU KISINDA KUSEPA YANGA

0

Usishtuke kabisa ukiona Yanga kwenye dirisha dogo la usajili wakamtambulisha kwa mara nyingine straika wao, Mburkinabe Yacouba Songne kwa sababu straika huyo yupo kamili kwa ajili ya kutumika tena.

Suala hilo linakuja baada ya Yacouba kupona kabisa majeraha yake ya goti ambayo yalimfanya kuachwa kwenye orodha ya wachezaji ambao wataitumikia timu hiyo msimu huu.

Ingawa nyota huyo haonekani kwenye kikosi cha timu hiyo lakini amekuwa akifanya mazoezi na kikosi hicho kambini Avic Town na kucheza katika baadhi ya michezo midogo midogo ya kirafiki kambini huko.

Mshambuliaji huyo amekaa nje kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu alipoumia katika mchezo wa Yanga dhidi ya Ruvu Shooting, mwanzoni mwa msimu ulipita.

Chanzo cha ndani kutoka Yanga kimesema kuwa, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi ameuomba uongozi wa timu hiyo kuangalia uwezekano wa kumrejesha Yacouba kutokana na ubora ambao amekuwa akiuonyesha mazoezini ambao ni zaidi ya baadhi ya wachezaji wengine wa kigeni ambao viwango vyao vimepungua kwa kiasi kikubwa kwa siku za hivi karibuni.

“Nabi ameonekana kuupenda uwezo ambao umekuwa ukionyeshwa na Yacouba Songne mazoezini, jambo ambalo tayari uongozi wa Yanga umeshapewa taarifa za Yacouba ili kuangalia uwezekano wa dirisha dogo akaingia ndani ya timu ili awe anacheza.

“Na kama ambavyo unafahamu kuwa Yanga tayari ilishakamilisha idadi rasmi ya wachezaji wa kigeni, jambo ambalo ni wazi kama viongozi watakuwa wamekubaliana na kocha juu ya ishu hiyo basi itabidi mchezaji mmoja wa kigeni aweze kumpisha dirisha dogo kisha aweze kupata nafasi ya kucheza.

“Kocha Nabi kuna baadhi ya wachezaji hafurahishwi nao kutokana na uwezo wao kushuka kwa sasa tofauti na awali, jambo ambalo ni wazi kuwa atahitaji kupata wachezaji kupitia dirisha dogo wa kuja kuongeza nguvu kwa ajili ya michuano ya kimataifa ambapo Yanga wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi,” kilisema chanzo hicho.

Katika kufahamu undani zaidi wa habari hiyo,  viongozi wa Yanga ambao wengi wao waliweka wazi kuwa akili zao ziilikuwa kwenye mchezo wao wa juzi wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar, ambao ulifanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here