Home KIMATAIFA KOMBE LA DUNIA QUATAR 2022: MABEKI VISIKI WA KUCHUNGWA

KOMBE LA DUNIA QUATAR 2022: MABEKI VISIKI WA KUCHUNGWA

0

DOHA. QATAR. KAZI ya beki ina changamoto kubwa sana kwani muda wote ni kumlinda kipa anapokuwa hatarini kufikiwa na adui. Vilevile beki ana kazi ya kuchuana vikali na mastraika wakali ambao ni wasumbufu wanapokuwa eneo lake ambao ni hatari kwa timu kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, Romelu Lukaku, Harry Kane, Alvaro Morata, Kylian Mbappe, Vinicius Juniour, Karim Benzema na wengine wengi watakaokutana na katika fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar kuanzia mwezi huu.

Wafahamu mabeki visiki wa kutazamwa watakaowakilisha mataifa yao katika fainali za Kombe la Dunia.

MARQUINHOS, ÉDER MILITÃO – BRAZIL

Marquinhos ni nahodha wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Brazil. Beki huyu amecheza kwa kiasi kikubwa ndani ya vikosi vya timu hizo. Katika fainali za Kombe la Dunia atakuwa na kazi ya kumsaidia kipa Alisson Becker akisimama eneo la beki wa kati akisaidiana na Eder Militao anayekipiga Real Madrid. Militao ana uwezo wa kucheza kama beki wa pembeni, lakini endapo kocha atapenda kumtumia katika nafasi tofauti. Militao ana kazi ya kuzuia mashamulizi kutokana na kasi yake. Anakaba na kuzuia mipira ya mwisho inayopigwa. Ni kati ya mabeki wazuri katika kikosi cha Brazil watakaokiwasha Qatar.

VIRGIL VAN DIJK, MATTHIJS DE LIGT – UHOLANZI

Uholanzi imepania kufanya vizuri katika fainali za Kombe la Dunia baada ya kukosa zile za 2018. Safari hii Uholanzi itakuwa chini ya kocha Louis van Gaal aliyewahi kukiongoza kikosi hicho na kukifisha nusu fainali ya Kombe la Dunia zilizofanyika 2014 nchini Brazil.

Katika nafasi za mabeki Van Gaal atawatumia Virgil Van Dijk anayekipiga Liverpool na Mattis De Ligt aliyejiunga na Bayern Munich dirisha la usajili la kiangazi mwaka huu akitokea Juventus. De Ligt (23) itakuwa michuano yake ya kwanza ya Kombe la Dunia. Beki huyo alikulia katika kituo cha kukuzia vipaji Ajax alikonolewa na kocha Erik ten Hag anayeinoa Manchester United kwa sasa. Mabeki hao ndio wataunda ukuta wa Uholanzi katika kipute cha Kombe la Dunia.

RÚBEN DIAS, JOÃO CANCELO – URENO

Ureno ilipata ilipambana kuhakikisha inafuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka huu. Licha ya kusuasua katika hatua ya makundi timu hiyo sio ya kubeza hasa ukizingatia ina mshambuliaji hatari ambaye pia ni nahodha wao, Cristiano Ronaldo anayekipiga Manchester United.

Ureno ina mabeki wazuri waliojipatia mafanikio Manchester City chini ya kocha Pep Guardiola. Mabeki hao walicheza kwa kiwango cha juu katika Ligi Kuu England pamoja na michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya. Kocha wa Ureno, Fernando Santos ni wazi atamtumia Dias mwenye uwezo wa kufunga na kukaba.

Kwa upande wa Cancelo anayecheza akitokea pembeni ana uwezo wa kutawala winga ya kushoto, ana nguvu na ubunifu wa kusaidia taifa lake katika fainali za Kombe la Dunia zitazofanyika Qatar na ndoto kubwa kwa upande wake kwani ni michuano ya kwanza kucheza na Dias.

LISANDRO MARTINEZ, NICOLAS TAGLIAFICO, NICOLAS OTAMENDI – ARGENTINA

Otamendi ana uzoefu ndani ya kikosi cha timu ya taifa ya Argentina. Amejumuishwa kikosini mara 92 katika historia ya soka lake kimataifa wakati Martinez amejumuishwa kikosini mara tisa. Martinez hii itakuwa ni mara ya kwanza kushiriki fainali za Kombe la Dunia tofauti na Otamendi. Martinez anayekipiga Manchester United ameonyesha kiwango bora tangu alipotua Ligi Kuu ya England baada ya kusajiliwa akitokea Ajax mwaka huu. Beki huyo ana nafasi kubwa ya kujumuishwa kikosini Argentina kutokana na uwezo wake wa kukaba akicheza sambamba na Otamendi mwenye uzoefu na michuano mikubwa ya kimataifa. Pia yupo beki mwingine wa Argentina, Nicolas Tagliafico anayetazamwa kwa jicho la karibu huku kocha wa taifa hilo, Lionel Scaloni akipata kigugumizi nani wa kuanza.

DAYOT UPAMECANO, PRESNEL KIMPEMPE – UFARANSA

Upamechano alionyesha kiwango bora katika michuano ya Nations League akiisaidia Ufaransa kubebwa ubingwa mwaka jana akicheza sambamba na Jules Kounde. Vilevile upande wa Kounde nafasi yake katika kikosi cha Ufaransa kitachoenda Qatar bado ni ndogo kutokana na majeraha yanayomsumbua tangu alijiunga na Barcelona mwaka huu. Ni wazi kwamba Upamecano anayekipiga Bayern Munich atapata nafasi katika kikosi cha Ufaransa pamoja na Kimpempe anayeichezea Paris Saint-Germain. Beki huyo hii itakuwa michuano yake ya pili kushiriki fainali hizo baada ya kuiongoza Ufaransa kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here