Mabosi wa Yanga wamemtega Gamondi wakimuachia nafasi ya kutafuta wasaidizi wake watatu katika benchi lake la ufundi wakiwemo kocha wa mazoezi ya viungo, kocha wa makipa na mtaalamu wa kuchambua mikanda ya wapinzani.
Nafasi hizo ziliachwa wazi kufautia kuondoka kwa Milton Nienov ambaye alikuwa kocha wa makipa, Helmy Gueldich aliyekuwa kocha wa mazoezi ya viungo na Khalil Ben Youssef aliyekuwa akifanya kazi ya kuchambua ubora wa timu pinzani kupitia mikanda ya video.
Gamondi anaweza kumkuta mwenyeji wake Cedric Kaze ambaye alikuwa msaidizi wa kocha aliyepita Nasreddine Nabi ambapo Mrundi huyo tayari ameshaonyesha hatua kubwa ya kukubali kuongeza mkataba ndani ya klabu hiyo.
“Kama ambavyo kocha aliyepita alikuja na watu wake na yeye (Gamondi) tumempa hiyo nafasi ashauri watu wa kuja nao tunachotaka awalete watu ambao watafanya kazi pamoja kwa ushirikiano siyo tumletee kisha baadaye wakaanza kupishana,” amesema mmoja wa mabosi wa Yanga aliyekuwa kwenye eneo zuri la maamuzi.
Hivi karibuni kocha mzoefu kwenye soka la Afrika ambaye ameshatwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu, Pitso Mosimane amesema “Siyo jambo zuri kumuajiri kocha mkuu halafu akaja akawakuta wasaidizi, ukimpa kazi mwambie aje na wasaidizi wake, huyu anaweza kufanya kazi nzuri zaidi kwa kuwa wanajuana kwenye tamaduni zao,”.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE