Home KITAIFA KISA KUTAKA KUJIUNGA SIMBA, BANGALA ‘AFOKEANA’ NA MABOSI YANGA

KISA KUTAKA KUJIUNGA SIMBA, BANGALA ‘AFOKEANA’ NA MABOSI YANGA

0

YANGA imekubali kiroho safi kuachana na Kocha Nasreddine Nabi. Lakini kimeibuka kitu kingine ambacho ni zaidi ya kivumbi na jasho na hakuna anayetaka kukitolea tamko.

Mastaa wao tegemeo watatu kutoka DR Congo, wameandika barua kuomba kusitisha mikataba yao na kuondoka klabuni hapo. Lakini viongozi wamenusa kwamba kuna mkono wa Simba na Azam kwenye muvu hiyo.

Gazeti la Mwanaspoti limejiridhisha na kuripoti kwamba Djuma Shaban, Lomalisa Mutambala na kiraka Yannick Bangala juzi kwa nyakati tofauti wamegonga mlango wa kutaka kuondoka na kwenye vikao vyao kulihusisha majibizano makali.

Djuma na Bangala ndio walianza ambapo wawili hao waliwasilisha ombi hilo la kusitisha mwaka mmoja wa mkataba wao baada ya kutumikia mwaka mmoja kwa mafanikio jangwani. Mikataba yao inaisha mwakani 2024.

Habari za uhakika ambazo zinafahamika ni kuwa wawili hao awali walipewa nusu ya ada ya usajili wao na katika miezi ya hivikaribuni wamekuwa wakifosi kumaliziwa bila mafanikio, hivyo wameambiana kwamba wasepe wakati huu wakatafute maisha pengine.

Katika hoja zao ni kwamba kile kiasi walichopewa awali ni cha muda waliofanya kazi kwahiyo kile wanachodai kitumike kusitisha mkataba sehemu iliyobaki jambo ambalo limeibua mjadala mzito ndani ya uongozi na hata kikao cha juzi hakikufikiwa muafaka.

Mabosi wa Yanga wamepata uhakika kwamba wakishafanya maamuzi hayo tu ndani ya siku mbili watani wao Simba na wapinzani wao Azam watashtua kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii kwamba ‘mgeni tumempata’.

Simba na Azam zinashindana kimyakimya kuisaka saini ya Bangala ambaye msimu mmoja uliopita alikuwa mchezaji bora wa ligi kwenda kuimarisha eneo lao la kiungo wa chini.

Yanga inajua kuna baadhi ya vigogo na wawakilishi wa klabu hizo wamekuwa wakifanya mazungumzo na Bangala na watu wao wa karibu wamevujisha siri.

Yanga imeshtukia hilo na wamemwambia Bangala kwenye kikao cha juzi jioni kwamba endapo anataka barua hiyo itakuwa na kipengele cha kumzuia kujiunga na timu yoyote ndani ya Tanzania jibu ambalo lilimfanya Mkongomani huyo kuwa mkali na kuanza kufoka.

Kinyume na sharti hilo Yanga ikamtaka Bangala kukubaliana na kupokea fedha iliyobaki ya usajili ili aendelee kutumikia mkataba wake sambamba na Djuma ambaye  anafosi ili aende Mazembe.

Jana mchana mabeki hao walitarajiwa kuwa na kikao kingine na mabosi wa Yanga katika kutafuta suluhu ya maombi yao, japokuwa imeelezwa kwamba ni ngumu haswa kutokana na kejeli ambazo Simba wameanza kuzitoa kwenye mitandao kwamba watatenganisha maji ya Bahari.

LOMALISA NA KISINDA

Yanga imepanga kuachana na Tuisila Kisinda ambaye atalazimika kurudi Morocco kwenye klabu yake ya Berkane, lakini Lomalisa naye mzuka umempanda anafosi kusepa nae. Wamemuwekea mkwanja mezani na akashawishika kuwasilisha maombi ya kutaka kuondoka Yanga.

Lomalisa inaelezwa ana ofa ya nchini Morocco kwa klabu ya RS Berkane lakini Yanga bado hawajaamini hilo wakiweka tahadhari ya kutoingizwa mkenge kama ule wa Bangala ambaye amekuwa mkimya lakini anafanya ishu zake chinichini.

Yanga imemwambia Lomalisa kama kuna timu inamtaka aipeleke mezani na watamlainishia safari ya kuondoka haraka ambapo kikao zaidi nacho kilitakiwa kuendelea jana japo uwezekano wa kumkubalia ni mdogo.

Kisinda yeye hana baya na mtu kwani anarejea klabu yake ya RS Berkane kwenda kumalizia mkataba wake wa mwaka mmoja, hilo lilikuwa kwenye mipango ya Yanga kwa muda kidogo.

Berkane imeridhika na kiwango chake katika mwaka mmoja alioitumikia Yanga kwa mkopo na sasa atarejea Morocco kumalizia mkataba wake ingawa hafurahii maisha ya nchi hiyo na uwezekano wa kudumu huko ni mdogo. Anatajwa kuwa kwenye mipango ya kujiunga na TP Mazembe na ameshawaambia waendelee na mazungumzo na Berkane.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here