Home KITAIFA PAMOJA SIMBA KUPATA BIL 4, UKWELI WOTE HUU HAPA KWA NINI VUNJA...

PAMOJA SIMBA KUPATA BIL 4, UKWELI WOTE HUU HAPA KWA NINI VUNJA BEI KAPIGWA CHINI

0

KLABU ya Simba imelamba dili nono ya Sh 4 Bilioni baada ya kuingia mkataba mpya wa miaka miwili wa makubaliano ya kutengeneza na kusambaza jezi na Kampuni ya Sandaland Fashion Wear Limited.

Mkataba huo umesainiwa jana jijini Dar es Salaam baada ya klabu hiyo kumalizana na Kampuni ya Vunja Bei iliyoingia nao miaka miwili iliyopita ukiwa na thamani ya Sh 2 Bilioni.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally, alisema kuwa, wameamua kuingia mkataba na Sandaland baada ya kuvutiwa na ofa yao iliyokuwa mara mbili na ile iliyopita ya Vunja Bei.

“Tunajivunia kwa kupata mkataba huu ambao utakuwa ni wa kutengeneza na kusambaza jezi za timu zetu. Ilikuwa ngumu kukataa ofa hii ya Sandaland na utakuwa wa miaka miwili na kila msimu itakuwa ni Sh 2 Bilioni, ikiwa na maana kwa miaka miwili klabu inavuna Sh 4 Bilioni,” alisema Ally.

Sandaland, ni moja ya kampuni ya Watanzania inayohusika na kuuza jezi ndani na nje ya nchi waliokuwa sehemu ya waliomba tenda, kampuni nyingine zikiwa ni Puma ya Afrika Kusini ambao nao walitoa ofa yao, lakini mabosi wa Simba wakavutiwa na kampuni hiyo.

Kulingana na mkataba huo, Sandaland wamepewa haki ya kuisimamia Simba kwenye matukio yake ya kimichezo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha mashabiki kununua jezi na kwenda uwanjani na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yusuf Omar Yenga aliwaahidi wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba kuwa watashuhudia jezi zenye ubora na zitakazopatikana kwa haraka kwani kwa sasa mzigo upo njiani unakuja.

“Tunawaahidi mashabiki kupata jezi zenye ubora na zitakazopatikana kwa wakati kabla hata ya Tamasha ya Simba Day, kwa vile mzigo kwa sasa upo njiani na tumejipanga kuusambaza mapema na kumfikia kila Mwanasimba,” alisema Yenga aliyefafanua wameanza kupokea oda za mawakala mikoani ili mzigo ukija usambazwe kuwawezesha wanasimba kupata jezi kirahisi popote alipo.

Yenga alisema Sandaland ina maduka makubwa mawili ya kuuza jezi jijini Dar es Salaam ambayo itawarahisisha wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba kupata jezi za msimu ujao kirahisi, huku wale wa mikoani watapata kwa mawakala watakaojiorodhesha na kuweka oda zao kuanzia sasa.

SABABU ZA VUNJA BEI KUPIGWA CHINI:

Aidha, taarifa za ndani kutoka kwa mabosi wa Simba, zinafichua kuwa sababu kubwa ya Fred Ngajiro kupitia kampuni yake ya Vunja Bei kunyimwa tena tenda hiyo ni pamoja na ucheleweshaji wa jezi, jezi kutokuwa bora huku pia ikibainishwa tabia ya Fred kuwavimbia mabosi wa klabu hiyo kulichochea.

Inaelezwa kuwa ukaribu wa Fred na Rais wa Heshima wa Simba, Ndg Mohammed Dewji ulimfanya kijana huyo mweye ukwasi kuona kwamba hakuna atakayemgusa.

Pia tulielezwa kuwa, kitendo cha kutoa ruhusa kwa wafanyabiashara wengine kariakoo kutengeneza jezi kwa kibali chake kiliwasonenesha wenye mamlaka ndani ya klabu hiyo.

Inaelezwa kuwa Fred aliwapa tenda wafanyabiashara wengine almaarufu kama ‘Wakinga’ kuchapisha jezi ambazo zilipkuja sokoni zilikuwa chini ya kiwango kile kilichokusudiwa.

Mbali na hivyo, sababu nyingine iliyopewa uzito wa sababu kuu ni dau aliloliweka , ambapo safari hii alitaka kuipa Simba Bilioni 1.5 kwa mwaka.

KUNA WALIOWEKA MZIGO MKUBWA ZAIDI YA SANDALAND.

Katika hali isiyoyakawaida, kitendo cha Sandaland the only one kupewa tenda ya kutengeneza jezi kiliwaacha kinywa wazi baadhi ya mabosi ndani ya klabu hiyo, kwani kwa dau alilolitoa kuna kampuni nyingine ya kitanzania iliweka dau kubwa zaidi ambapo hawakupewa nafasi.

Tumeelezwa kuwa , Kampuni hiyo ‘jina kapuni’ iliwasilisha ofa ya Bilioni tatu kasoro kwa mwaka mmoja pamoja na mambo mengine mengi ambayo watafanya.

Kampuni hiyo ilijikuta ofa yake inatupwa mbali kwa kile kilichoelezwa kuwa ni wageni miongoni mwa macho ya watanzania, huku pia ukaribu baina ya Sandaland na baadhi ya mabosi wa timu hiyo ukiifanya Sandaland the only one kupewa tenda hiyo.

SIO JEZI TU, HADI JENGO KAPEWA:

Jana mara baada ya tukio hilo kuisha, Mwenyekiti wa Simba upande wa mashabiki Ndg Murtaza Mangungu alifichua kuwa Sandaland pia wamekodishwa majengo ya msimbazi kuyaendesha kibiashara.

Mangungu alisema hayoa mara baada ya kuulizwa na mtangazaji wa Azam TV kuhusu uhakika wa Simba kufanya kazi na Sandaland, ambapo alisema kuwa wanamuamini kwani hata majengo yao ya msimbazi ni yeye anayeyasimamia kwa sasa.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here