Simba imemaliza msimu wa 2022-2023, bila taji lolote na kinachoendelea kwa sasa ni vikao vya mara kwa mara kwa mabosi wa klabu hiyo kwa lengo la kupanga mikakati ya kusuka kikosi kikali kwa msimu ujao, huku ikielezwa kiungo Ismael Sawadogo na winga Peter Banda wakiwagawa mabosi hao.
Ipo hivi. Mabosi wa Simba wamekuwa kwenye vikao mfululizo vya Bodi ya Wakurugenzi chini ya Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again’, huku mada kubwa ikiwa ni usajili wa wachezaji wapya sambamba na wanaoachwa kutokana na kushindwa kufanya vizuri.
Hata hivyo vigogo hao waligawanyika kwenye ishu ya kuwapiga chini Banda anayetakiwa na Azam ambaye amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja, sambamba na kiungo Mburkina Faso, Ismael Sawadogo, huku baadhi ya wachezaji wakipigiwa hesabu za kupelekwa West Armenia.
Sawadogo na Banda wote bado wana mkataba wa mwaka mmoja na Simba ambapo kwa Sawadogo wako tayari kuuvunja lakini inaonekana watatakiwa kumlipa pesa ndefu huku kwa Banda viongozi wakigawanyika kuhusu kumuacha.
Wapo wanaoamini Banda ana kipaji kikubwa na umri wake unamruhusu kuendelea kucheza Simba wakiwa na matumaini ya winga huyo kufanya vizuri kwenye misimu ijayo lakini pia wapo wanaodhani ni muda wake kuondoka kwani ameshindwa kuonyesha muendelezo wa kiwango chake katika muda aliokaa Simba na amekuwa na majeraha ya mara kwa mara.
Hata hivyo, uongozi wa Simba upo tayari kupokea ofa ya timu yeyote itakayohitaji huduma ya wawili hao kwa mkataba wa mkopo ama kununuliwa jumla. Ripoti zinaeleza Azam ni miongoni mwa timu zinazovutiwa kumsajili Banda.
Endelea kutembelea www.sokaleo.com kwa habari mbali mbali za kimichezo
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE