Home KITAIFA KIMEUMANA YANGA, MUSONDA AITAKA NAFASI HII YA MAYELE

KIMEUMANA YANGA, MUSONDA AITAKA NAFASI HII YA MAYELE

0

Wakati msimu mpya ukianza na kitendawili cha nani atakuwa mrithi wa mshambuliaji Fiston Mayele, nyota wa Yanga, Kennedy Musonda amefunguka akisema anaitaka nafasi ya mfungaji huyo bora wa msimu.

Mayele aliibuka na tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mara 17, sawa na nyota wa Simba, Saidi Ntibazonkiza, huku pia akiwa kinara wa ufungaji katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mabao saba.

Musonda, ambaye tangu atue Yanga amekuwa akitumika kama winga, huku mara moja pekee akipewa nafasi ya kuanza kama mshambuliaji wa kati, alisema yuko tayari kutumika nafasi yoyote ambayo kocha Miguel Gamondi atahitaji acheze.

Musonda alisema licha ya utayari wake huo, lakini kama kuna nafasi anatamani kuicheza uwanjani na anakuwa huru ni kucheza kama mshambuliaji wa kati, ambayo alikuwa akiitumia Mayele.

“Mimi siwezi kukataa uamuzi wa kocha atakapotaka nicheze, nitacheza tu kama ambavyo nimekuwa nikifanya sasa, lakini kwangu binfasi napenda kutumika kama namba tisa.

“Huwa najiona niko huru sana nikicheza hapo, lakini kikubwa napenda kufunga, hata msimu ujao nimejipanga kufunga sana kila nitakapopata nafasi ya kucheza,” alisema nyota huyo.

Msimu uliopita, moja ya mechi ambayo Musonda alitumika kucheza kama namba tisa ilikuwa kwenye fainali ya Kombe la FA (ASFC), akifunga kwa kichwa bao pekee lililoipa Yanga ubingwa wa mashindano hayo.

Msimu huu, katika mchezo wa kwanza kwenye kilele cha Mwananchi, wakati Yanga ikiifunga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini bao 1-0, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Zambia alifunga tena bao pekee la mchezo huo, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni alisema hawezi kumfananisha Musonda na Mayele, kwani wana ubora na uwezo tofauti.

Kibadeni alisema kupata mtu kama Mayele ni ngumu kwa wakati huu, kwa sababu hakuna uhakika wa hao waliokuja au waliobaki kama watafanya kama alichokifanya nyota huyo wa kimataifa wa DR Congo.

“Rekodi zake ni kubwa na inatuhitaji mechi tatu au msimu mzima ili kumfahamu kama mrithi kapatikana au ndioi tuishi na kumbukumbu tu.

“Musonda anakazi ya ziada kutuaminisha kuwa anauwezo wa kufanya yale yaliyofanywa na mshambuliaji aliepita kwangu naweza kusema bado sijaona mrithi,” alisema Kocha wa zamani wa Simba Kibadeni.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here