Home KITAIFA MSHAHARA WA LUIS MIQUISSONE HAPO SIMBA NI KUFURU

MSHAHARA WA LUIS MIQUISSONE HAPO SIMBA NI KUFURU

0
Luis Miquissone

WAKATI kundi la mwisho la wachezaji wa Simba likijianda kupaa jana kwenda kambini Ankara, Uturuki, winga anayerejeshwa Msimbazi kutoka Al Ahly ya Misri, Luis Miquissone anatajwa kufunika kwa dau la mshahara atakaokuwa analipwa kikosini.

Luis aliyeuzwa na Simba misimu miwili iliyopita kwa Al Ahly inaelezwa dili lake limekamilika la kurudi katika klabu hiyo, huku ikielezwa amewekewa fedha za maana za usajili sambamba na mshahara atakaokuwa akilipwa akiwafunika wachezaji wengine.

Ndio! Kwa sasa ni rasmi Luis aliyeuzwa na Simba misimu miwili baada ya kufanya makubwa aliposajiliwa kutoka UD Songo ya Msumbiji, atavaa uzi mwekundu na mweupe wa Mnyama kama aliokuwa akivaa Al Ahly, baada ya klabu ya sasa kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.

Soka la bongo ambalo ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti kurudi kwa staa huyo kabla ya klabu yake kuthibitisha kuvunja mkataba, liliwajulisha jana kwamba dili hilo lilikuwa limefikia patamu na jana limejiridhisha mchezaji huyo ataichezea Simba msimu ujao baada ya kukamilisha kila kitu ili kurudi Msimbazi.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinadai kwamba winga huyo ndiye atakuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi kwani dili lake ni la Dola 120,000 (zaidi ya Sh240 milioni), huku akivuta mshahara wa Sh34 milioni kwa mwezi.

Mabosi wa Simba wamethibitisha kwamba, tayari wamempa Luis mkataba wa miaka miwili na anatarajiwa kuungana na Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kuanzia leo, Alhamisi pamoja na wenzake kambini Uturuki.

Mmoja wa vigogo wa Simba (jina tunalo), ameliambia Mwanaspoti kuwa winga huyo hatima yake ni wiki hii lengo likiwa ni kuona timu hiyo inafikia malengo ndani na nje kwenye mashindano inayoshiriki.

Luis aliyesajiliwa na Simba 2020 akitokea UD Songo ya Msumbiji hadi anaondoka Msimbazi miaka miwili iliyopita alikuwa amefunga mabao tisa na asisti 15 na sasa anarejea Simba akitokea Abha aliyokuwa akiichezea kwa mkopo baada ya kutolewa na Al Ahly.

“Luis ni mchezaji huru sasa hakuna asiyefahamu na kila kona anatajwa kuhusishwa na Simba ambao ni waajiri wake wa zamani. Hatutaki kuzungumza mengi lolote linaweza kutokea na hatima yake kama ni mchezaji wa Simba itakuwa ndani ya wiki hii,” alisema kigogo huyo.

“Kambi ya Uturuki itanoga, itakuwa na wachezaji wote wapya na wa zamani, hivyo kama ni miongoni mwao, basi itajulikana kwa sababu atatakiwa kuungana na wenzake hukohuko Ankara.”

Kutua kwa Luis kunaifanya Simba iongeze nguvu eneo la mbele ambalo tayari lina maingizo mawili mapya akiwamo Aubin Kramo kutoka Asec Mimosas ya Ivory Coast na Willy Onana aliyekuwa Rayon Sports ya Rwanda na jana ilimtambulisha Fabrice Ngoma aliyekuwa Al Hilal ya Sudan.

Mbali na hao, Simba kikosini ina Kibu Denis, Peter Banda, Moses Phiri, John Bocco, Saido Ntibazonkiza na Pape Sakho aliye mbioni kuondoka kwenda Ufaransa.

Katika hatua nyingine, Simba imenasa mrithi wa Jonas Mkude baada ya kunasa saini ya kiungo Mtanzania aliyekuwa Tusker ya Kenya, Hamis Abdallah.

Simba ambao katika nafasi ya kiungo wana wazawa wawili Mzamiru Yassin na Nassoro Kapama ilhali upande wa wageni ni Sadio Kanoute na Willy Onana.

Ujio wa Hamis utaongeza chachu ya ushindani kwenye eneo hilo huku kiungo huyo akiwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha anapata namba mbele ya Mzamiru ambaye amejitengenezea ufalme katika kikosi cha kwanza.

“Usajili wa kiungo huyo ni mapendekezo ya kocha ambaye aliomba kila nafasi kuwa na wachezaji wawili ili kuwa na kikosi cha ushindani.

“Tayari mchezaji huyo amekamilisha usajili na atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaoitumikia Simba msimu ujao. Tunaamini ongezeko lake litakuwa na chachu ya ushindani,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina litajwe gazetini.

Chanzo kimethibitishiwa kuwa usajili upande wa wazawa umekamilika ka mujibu wa ripoti ambayo ilikuwa inahitaji wachezaji watatu ambao hadi sasa wamekamilika.

Wachezaji wazawa waliosajiliwa dirisha hili la usajili ni mshambuliaji Shaban Chilunda, Hussein Bakari ambaye ni beki wa kati na Hamis katika nafasi ya kiungo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ kwenye mazungumzo ya hivi karibuni alisema bado wanaendelea kufanya usajili mzuri na bado kuna vifaa vingine vitatambulishwa hivi karibuni.

“Wachezaji wapya wanaendelea kuwasili kambini. Nawakumbusha tu hatujamaliza kusajili furaha zaidi itakuja hivi karibuni,” alisema Try Again.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here