WAKATI Simba ikipambana dhidi ya Singida Fountain Gate jukwaani kulikuwa na ugeni wa watu wanne wakiwasoma ambao uwepo wao hapo hauna habari njema kwa wekundu kutokana na chabo waliyokuwa wakipigwa na ugeni huo kutoka Yanga.
Jukwaani kulikuwa na makocha wanne wa Yanga kuanzia kocha mkuu Miguel Gamondi na wasaidizi Mussa Ndaew, kocha wa viungo Taibi Langrouni na kocha wa makipa Aaal Maskini wakiwasoma wapinzani wao.
Gamondi hakuwahi kuishuhudia Simba tangu aje nchini na juzi akapata nafasi akiwasoma vizuri wapinzani wake hao ambao watakutana nao kwenye fainali ya kuwania Ngao ya Jamii kesho Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Wakati Gamondi akiwa jukwaani, mashabiki wa Simba walikuwa wakimtupia vijembe lakini wenyewe wala walikuwa hawasumbuki na hilo kwa kuwa hawakuwa wanaelewa lugha hiyo waliyokuwa wanaitumia.
Muda mrefu makocha hao walikuwa wakiandika vitu mbalimbali kwa kutumia simu zao za mkononi kwa kile walichokiona katika mchezo huo uliokuwa mgumu ukimalizika kwa dakika 90 bila bao kisha kwenda kwenye penalti na Simba kushinda 4-2. Mara baada ya mchezo Gamondi alitoka mara tu Simba ilipopata penalti ya mwisho, iliyopigwa na Moses Phiri, huku akionekana akicheka na wasaidizi wake.
Kocha huyo hakutaka kuongea lolote baada ya kumalizika mchezo ambapo waliondoka haraka uwanjani wakiwa kwenye ulinzi mkali wa walinzi wa timu yao maarufu kwa jina la Task Force.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE