Home MAKALA MSIMU UNAANZA, WAAMUZI MSIJIFICHE KWENYE MAKOSA YA KIBINADAMU

MSIMU UNAANZA, WAAMUZI MSIJIFICHE KWENYE MAKOSA YA KIBINADAMU

0
waamuzi

KUNA rundo la lawama wamekuwa wakiangushiwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na watu wazembe ambao hufanya mambo kwa maslahi yao binafsi.

Waamuzi wamekuwa kati ya wale wanaosababisha TFF kuangushiwa lawama nyingi sababu tu ya uzembe wanaofanya.

Najua, imekuwa si kawaida kuwaona wadau wakiwasifia TFF kutokana na utendaji mzuri wa waamuzi, ni hadi pale wanapoharibu tu!

Hili ni kawaida lakini kwa sasa ni wakati mwafaka wa kukumbushana kuwa tunakwenda kuuanza msimu mpya wa 2023/24.

Tanzania kwa sasa imepata hadhi ya juu kupitia mchezo wa soka na Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC Bank ni kati ya ligi bora tano barani Afrika.

Lazima tukubali kufikia hapo haikuwa kwa ndoto yaani kulala na kuamka tukiwa tumefika. Kila upande unaohusika na udau uliifanya kazi yake vizuri.

TFF imeifanya kazi yake kwa ubora wa juu. Suala la usimamizi wa mambo limekuwa juu na ndio maana unaona mafanikio yamekuwa bora.

Ligi kufikia hatua hiyo, kwanza ni lazima tuwapongeze waamuzi kuwa wamekuwa sehemu ya waliochangia kupigwa kwa hatua na kufikia hapo.

Si waamuzi wote wamekuwa wakiboronga kwa makusudi kwa ajili ya maslahi yao binafsi na baadaye wakasingizia kuwa yalikuwa ni makosa ya kibinadamu.

Kama ingekuwa hivyo, maana yake tungekuwa hatujapiga hatua hii tuliyofikia kwa kuwa lazima tukumbuke waamuzi ni watu muhimu sana.

Kila wanapoifanya kazi yao ya kutafsiri sheria 17 za mchezo wa soka kwa ufasaha, basi wanakuwa wanatengeneza ubora wa mchezo wa soka kwa kuwa wanazalisha ushindani chanya ambao unam ashiko ya mafanikio.

Kuna suala la makosa ya kibinadamu limekuwa likitumika vibaya sana. Yako makosa ya makusudi kabisa, yamekuwa yakifanywa na baadhi ya waamuzi ambao tafsiri sahihi huwa ni makosa ya kimaslahi.

Tunajua katika mchezo kama wa soka, hakuwezi kukosekana kwa makandokando ambayo yanakuwa tatizo kubwa kwenye mpira wa Tanzania.

Kusema hakuna rushwa kabisa itakuwa ni kujidanganya lakini inawezekana kuna ugumu wa kupatikana au kushikwa kwa washiriki wa tendo hilo kwa kuwa wanaotoa na wanaopokea wamekuwa wakikubaliana au kuifurahia hali hiyo.

Pamoja na kwamba wanafurahia, binafsi naendelea kuwakumbusha kwamba wanachofanya ni rahisi kugundulika kwa kuwa mpira unachezwa hadharani.

Penalti za dhuluma, kadi za uonevu na kadhalika yamekuwa ni sehemu ya matokeo yanayotokana na uamuzi wa waamuzi wenye maslahi binafsi.

Kweli kama binadamu, mwamuzi anaweza kukosea lakini angalau kunaweza kuwa katika kiwango ambacho kinasoma kuwa mwamuzi yule alifanya kosa la kibinadamu lakini wakati mwingine uhalisia unakataa.

Pia mwamuzi mmoja, hawezi kuwa na makosa mengi yaliyopindukia ya kibinadamu ambayo yanapelekea kwenye uzembe au makusudi.

Makosa mengi humfanya mtu aonekane si makini, kukosa umakini kunakufanya kupoteza sifa za kuaminika na kama hauaminiki maana yake hauna sifa.

Hapa ninachogusa kuwa lazima watu wanaopewa dhamana ya kuchezesha wajue wanabeba dhamana kubwa ya mchezo wa soka ambao uko chini ya Watanzania.

TFF wanapata shida kwa kuwa wao wamepewa hiyo dhamana lakini nao wanapochukua hatua kali basi tuwaunge mkono.

Maana wanaokosea ndio wamekuwa wanasababisha huu uharibifu kwa maslahi yao. TFF wakisimama na wakawa imara basi taratibu wataondoka.

Mwishoni mwa msimu uliopita kulikuwa na ukimya mkubwa. Hii ikitokana na idadi kubwa ya waamuzi waliokuwa wanaboronga kuondolewa kimyakimya.

Wale wapya wakaingia na kuifanya kazi yao kwa ufasaha na ndio maana uliona mambo yakatulia kabisa.

Lazima tukubali kila mmoja akifanya kazi yake kwa ufasaha na hasa kwa waamuzi, mambo yataenda kwa usahihi na kutakuwa na ushindani sahihi.

MUHIMU:Picha haina uhusiano na kilichoandikwa katika makala haya.

HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here