ADHABU ya kifungo cha mwaka mmoja ipo juu ya Hassan Mwakinyo, ambaye amefungiwa kupanda ulingoni kwa muda huo.
Mbali na kifungo hicho anapaswa kulipa faini ya shilingi milioni moja, kwa kosa la kugoma kupanda ulingoni katika Usiku wa Viwango, Septemba 29 2023.
Uamuzi huo umefanywa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa nchini (TPBRC) kupitia kamati yake ya nidhamu baada ya kusikiliza pande zote mbili, yaani upande wa bondia Hassan Mwakinyo na upande wa promota wa pambano lile, PAF Promotion.
Akitangaza uamuzi huo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TPBRC, George Silas amesema kamati imefikia uamuzi huo baada ya kuona sababu za Mwakinyo kutopanda ulingoni, hazina mashiko kwakuwa zilikosa vielelezo.
“Baada ya kusikiliza pande zote tumeona kuwa sababu za bondia Hassan Mwakinyo hazikuwa na mashiko hivyo hakufuata taratibu kwenye kugomea pambano hilo,”.
Bondia Hassan Mwakinyo alitakiwa kupigana na Julius Indonga lakini saa 12 kabla ya pambano hilo alitangaza kutopigana akitaka kampuni ya Mafia Boxing (iliyokuwa sehemu ya wadhamini) isihusishwe kwenye tukio hilo.
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE