Kambi ya Simba mzuka umepanda zikiwa zimebaki siku nne tu kabla ya timu hiyo kushuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuvaana na Al Ahly katika mechi ya uzinduzi wa Ligi mpya ya Afrika ‘African Football League’, huku kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akifichua hiyo ni mechi ya Aishi Manula.
Kocha Robertinho ameliambia Mwanaspoti ameridhishwa na kiwango cha Manula na moja kwa moja ameamua kumuweka kwenye mipango ya mchezo huo wa Ijumaa “Kila kocha anatamani kuwa na wachezaji wote kikosini, tumefurahi kumwona Manula akirejea lakini kwa kuonyesha kiwango bora. Kitu kizuri amerejea wakati tukijiandaa na mechi ya Al Ahly, ni mchezaji mzoefu na tayari tumemjumuisha kwenye mipango yangu kama ilivyo kwa wengine,”
Baadhi ya wadau wamezungumzia juu ya kurejea kwa Manula na kusema itakuwa na faida kwa timu kwani tangu kipa huyo alipoumia, kulikosekana utulivu kwenye eneo hilo licha ya kuwepo kwa makipa wengine na mabeki waliokuwa na kazi kubwa ya kuwalinda iwe katika mechi za ndani na zile za kimataifa.
Nyota wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amesema; “Manula ni mkongwe na mzoefu kwa mechi ngumu kama hii, japo sidhani kama atakuwa na utimamu wa mechi (Game Fitness) kwa kiwango kikubwa, ila benchi la ufundi ndilo lina maamuzi,” alisema Julio na kuongeza;
“Hata asipodaka Manula, makipa wengine waliopo Simba wanaweza kudaka na kufanya vizuri, hakuna kipa asiyefungwa duniani, hivyo Simba inachotakiwa kufanya ni kucheza kwa tahadhari na kupunguza makosa kwenye kila eneo.”
Kiungo wa zamani wa Tukuyu Stars, Yusuph Kamba ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka amesema; “Ni jambo jema kuona amerejea katika majukumu yake. Uwepo wake kikosini utaleta hamasa hata kwa wachezaji wengine pia wataongeza hali ya kujiamini kwani ni mzoefu pia akiwa langoni ni kama kiongozi kwa mabeki wake.”
HABARI HIZI ZINAPATIKANA KATIKA APP YETU YA SOKALEO >>BONYEZA HAPA<<< KUIDOWNLOAD PLAYSTORE